TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo imepewa dhamana ya kuendesha mchakato wa Ajira kwa niaba ya waajiri mbalimbali Serikalini, imeendelea kuboresha na kurahisisha mchakato wa Ajira kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA katika kutangaza nafasi za kazi, kupokea maombi, kuwaita kwenye usaili na kuwapa wadau taarifa mbalimbali za kazi pamoja na kuwawezesha waombaji kazi kutumia teknolojia kupata Ajira, Katika kuwawezesha wananchi hususan waombaji fursa za Ajira kupata taarifa za Ajira kwa wakati na uhakika, Sekretarieti ya Ajira pamoja na kutumia tovuti yake ya www.ajira.go.tz imeanzisha mifumo mingine miwili ya kielekroniki ili kuhakikisha kuwa maombi yote ya fursa za Ajira yanapokelewa na taarifa mbalimbali kuhusu Ajira zinawafikia Watanzania wengi zaidi hususan wanaoishi vijijini na nje ya mipaka ya nchi yetu.
Mifumo hiyo ni pamoja; Mfumo wa kuomba fursa za Ajira unaojulikana kama “recruitment portal” na unapatikana kwa anuani “portal.ajira.go.tz” na mfumo wa pili ni kwa ajili ya kupata ujumbe mfupi wa fursa za Ajira za papo kwa papo kupitia simu za kiganjani ujulikanao kama “Job alert system” na unaweza kuupata kwa kubofya *152*00# na kufuata maelekezo. Sababu za kuanza kutumia mifumo hii zinalenga kupunguza changamoto kadhaa zikiwemo Malalamiko ya baadhi ya waombaji fursa za Ajira kuhusu upotevu wa maombi yao ya kazi, Mchakato wa Ajira kuchukua siku nyingi ili kukamilika (Takribani siku 90 zilitumika kukamilisha mchakato mzima wa Ajira), Namna ya kuzihifadhi taarifa zote za waombaji fursa za Ajira na kazi ya rejea pale kunapokuwa na haja ya kufanya hivyo, Kupunguza gharama za kuendesha mchakato wa Ajira na mwisho ni kuhakikisha tunapanua wigo wa utoaji taarifa za uwepo wa fursa za Ajira hasa kwa waombaji fursa za Ajira waishio vijijini.
Mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kutumika kwa mifumo hii: Mfumo wa utumaji maombi ya kazi kwa njia ya kieletroniki (recruitment portal) umekuwa na manufaa makubwa ambapo umeweza kupunguza muda wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira kutoka siku 90 hadi siku 52 kwa sasa. Pia mfumo huu umesaidia waombaji wa kazi kuwa na uhakika wa maombi yao kupokelewa kwa wakati na kupata mrejesho wa papo tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo maombi ya kazi yalikuwa yakipokelewa. Mfumo wa “Job alert” kwa kutumia simu za kiganjani umeongeza idadi kubwa ya waombaji wa fursa za Ajira na umerahisisha taarifa za fursa za Ajira kufika maeneo mengi zaidi, kwa kuwa kinachotakiwa ni mhusika kuwa na simu na kujisajili katika mfumo atapata taarifa za kazi zilizotangazwa na Serikali wakati huo.
Hadi kufikia tarehe 29 Mei, 2016, jumla ya waombaji wa fursa za Ajira waliojiandikisha kwenye mfumo wa utumaji maombi ya kazi walikuwa (97,765). Aidha, jumla ya waombaji wa fursa za Ajira (89,484) wamejiunga kwenye mfumo wa kupata taarifa za uwepo wa fursa za Ajira kupitia simu za kiganjani na barua pepe. Mwisho; Sekretarieti ya Ajira inatoa Rai kwa waombaji fursa za Ajira kujisajili katika mfumo wa Ajira unaopatikana kupitia anuani portal.ajira.go.tz na mfumo wa “Job alert system” kwa kubofya *152*00# ili kuweza kuomba fursa za ajira zinapopatikana. Tunawahimiza wale wote ambao hawajajiunga na mfumo huu hasa wahitimu wa Vyuo mbalimbali, kufanya hivyo maana mfumo huu ndio njia pekee inayotumika kupokelea maombi ya kazi kwa michakato yote inayoendeshwa na Sekretarieti ya Ajira.
Chanzo CLICK HERE
No comments:
Post a Comment