15 November, 2012

CHANGAMOTO KUBWA KWA SUMATRA

Ni wazi kwamba suala la usafiri hususani ule usafiri wetu wa umma bado ni kero kubwa katika nchi yetu. Hali hii inatokana na ubovu wa miundombinu, ama mamlaka husika kutowajika ipasavyo au yote kwa pamoja
.
Hapa najaribu kuangazia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) ambao ndio wenye dhamana hiyo. Kuna hii kasumba ya daladala nyingi kukatisha au kubadili ruti na kupandisha nauli nyakati za jioni hususani katika jiji la Dar es Salaam,,mfano wale wanaokaa kimara,mbezi Louis washaitwa sana kama 'mawe' (mawe/jiwe ni abiria ambaye anapanda basi mwanzo wa basi mpaka mwisho wa basi bila kushuka na ukitoka k/koo utaambiwa gari inaishia manzese au lipa 1000 kimara hali ambayo kwa sasa imeshazoeleka na kuwa kama kitu cha kawaida. Ukiachilia mbali daladala,kuna mabasi yaendayo mikoani kujipandishia nauli kiholela hasa kuanzia mwezi novemba, desemba hadi januari

.
Kwa kawaida kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na mwaka mpya, watu wengi husafiri kwenda maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya kujumuika na ndugu na jamaa zao, hapo ndipo wasafirishaji huona wamepata fursa ya kujineemesha maradufu isivyo halali. Sasa hivi tayari zimeshaanza kuonekana dalili za nauli kupanda kwa zaidi ya asilimia 15 ya nauli ya kawaida. Mathalani nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya baadhi ya mabasi inasemekana imeshafikia tshs 32,000 hadi 35,000 badala ya tshs 28,000-30,000 nauli ya kawaida

.
Nashindwa kuelewa hawa SUMATRA wanafanyaje katika kuwadhibiti hao wenye mabasi wanaojipa mamlaka ya kujipandishia nauli kwa sababu tu ya tamaa zao na kuwaathiri watumiaji wa usafiri huo. Nakumbuka kuna wakati fulani maafisa toka SUMATRA walikuwa wakifanya ukaguzi wa kushitukiza katika vituo vikuu vya mabasi hasa pale Ubungo. Walikuwa wanaingia kwenye mabasi hayo na kuzikagua tiketi za abiria ambapo wakibaini kuwa nauli iliyotozwa si halali, wenye mabasi walikuwa wakichukuliwa hatua stahili ikiwa ni pamoja na kuamuriwa wawarudishie abiria pesa zao zilizozidi katika nauli ya kawaida.
Lakini shida iliyopo ni kwamba operesheni za namna hii inaonekana ni kama 'nguvu ya soda' ndio maana tatizo huwa linajirudia na kujirudia.


SUMATRA kwa kushirikiana na mamlaka zingine husika wanapaswa kulivalia njuga suala hili, maana kwa jinsi inavyoonekana hii KAZI YAO SI RAHISI kama vile wanavyoichukulia. Ingefaa ule utaratibu wa kufanya ukaguzi wa tiketi liwe ni zoezi la kudumu badala ya kufanya kwa kushitukiza kisha kukaa kimya tena, hali inayowapa mwanya wenye mabasi kujiamulia watakavyo wao na hivyo kuzidi kuwaumiza wasafiri ambao hawana hatia yoyote.Pia abiria waache mtindo wa kununua tiketi vichochoroni badala ya kununua katika ofisi ya basi husika.Ijulikane wazi kua SUMATRA pekee yao bila ushirikiano na wenye mabasi pamoja na abiria haitaweza  baini matatizo/changamoto ambazo zinakua  sugu siku hadi siku

No comments: